Mark 7

Kilicho Safi Na Kilicho Najisi

(Mathayo 15:1-20)

1 aMafarisayo na baadhi ya walimu wa sheria waliokuwa wametoka Yerusalemu wakakusanyika mbele ya Isa. 2 bWakawaona baadhi ya wanafunzi wake wakila chakula kwa mikono iliyo najisi, yaani, bila kunawa kama ilivyotakiwa na sheria ya dini ya Wayahudi. 3 cKwa kuwa Mafarisayo na Wayahudi wote hawali chakula pasipo kunawa kwa kufuata desturi za wazee wao. 4 dWanapotoka sokoni hawawezi kula pasipo kunawa. Pia kuna desturi nyingine nyingi wanazofuata kama vile jinsi ya kuosha vikombe, vyungu na vyombo vya shaba.

5 eKwa hiyo wale Mafarisayo na walimu wa sheria wakamuuliza Isa, “Mbona wanafunzi wako hawafuati desturi za wazee, na badala yake wanakula kwa mikono najisi?”

6 fIsa akawajibu, “Nabii Isaya alisema ukweli alipotabiri juu yenu, ninyi wanafiki. Kama ilivyoandikwa: “ ‘Watu hawa huniheshimu kwa midomo yao,
lakini mioyo yao iko mbali nami.

7 gHuniabudu bure,
nayo mafundisho yao ni maagizo ya wanadamu tu.’

8 hNinyi mmeziacha amri za Mungu na kushika desturi za watu.”

9 iNaye akawaambia, “Ninyi mnayo njia nzuri ya kukataa amri za Mungu ili mpate kuyashika mapokeo yenu! 10 jKwa mfano, Musa alisema, ‘Waheshimu baba yako na mama yako,’ na, ‘Yeyote amtukanaye baba yake au mama yake, na auawe.’ 11 kLakini ninyi mwafundisha kwamba mtu akimwambia baba yake au mama yake, ‘Kile ambacho ningeweza kukusaidia ni Korbani’ (yaani kimewekwa wakfu kwa Mungu), 12basi hawajibiki tena kumsaidia baba yake au mama yake. 13 lKwa njia hiyo ninyi mnabatilisha neno la Mungu kwa mapokeo yenu mliyojiwekea. Nanyi mnafanya mambo mengi ya aina hiyo.”

14 mIsa akaita tena ule umati wa watu, akawaambia, “Nisikilizeni, kila mmoja wenu na mwelewe jambo hili. 15 nHakuna kitu kinachomwingia mtu kimtiacho unajisi, lakini kile kimtokacho ndicho kimtiacho unajisi. [ 16 oKama mtu yeyote ana masikio ya kusikia na asikie.]”

17 pAkiisha kuuacha ule umati wa watu na kuingia ndani, wanafunzi wake wakamuuliza maana ya mfano ule. 18Akawajibu, “Je, hata nanyi hamwelewi? Je, hamfahamu kwamba kitu kimwingiacho mtu hakimtii unajisi? 19 qMtu akila kitu hakiingii moyoni mwake bali tumboni, na baadaye hutolewa nje ya mwili wake.” (Kwa kusema hivi, Isa alivihalalisha vyakula vyote kuwa ni “safi.”)

20Akaendelea kusema, “Kile kimtokacho mtu ndicho kimtiacho unajisi. 21 rKwa maana kutoka ndani ya moyo wa mtu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wizi, uuaji, uzinzi, 22 stamaa mbaya, uovu, udanganyifu, ufisadi, wivu, matukano, kiburi na upumbavu. 23Maovu haya yote hutoka ndani ya mtu, nayo ndiyo yamtiayo mtu unajisi.”

Imani Ya Mwanamke Msirofoinike

(Mathayo 15:21-28)

24 tNdipo Isa akaondoka hapo akaenda sehemu za Tiro. Akaingia katika nyumba moja, naye hakutaka mtu yeyote ajue kwamba yuko humo. Lakini hakuweza kujificha. 25 uMara mwanamke mmoja, ambaye binti yake mdogo alikuwa na pepo mchafu, akaja na kumpigia magoti miguuni pake. 26Basi huyo mwanamke alikuwa Myunani, aliyezaliwa Foinike ya Siria.
Kulikuwa na Foinike ya Siria (ndio Shamu) na Foinike ya Libya.
Akamsihi Isa amtoe binti yake huyo pepo mchafu.

27Isa akamwambia, “Waache watoto washibe kwanza, kwa maana si vyema kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.”

28Lakini yule mwanamke akamjibu, “Bwana, hata mbwa walio chini ya meza hula makombo ya chakula cha watoto.”

29Ndipo Isa akamjibu, “Kwa sababu ya jibu lako, nenda zako nyumbani; yule pepo mchafu amemtoka binti yako.”

30Akaenda zake nyumbani akamkuta binti yake amelala kitandani, yule pepo mchafu akiwa amemtoka.

Isa Amponya Mtu Aliyekuwa Kiziwi Na Bubu

31 wKisha Isa akaondoka sehemu za Tiro, akapita katikati ya Sidoni, hadi Bahari ya Galilaya na kuingia eneo la Dekapoli. 32 xHuko, watu wakamletea Isa mtu mmoja kiziwi, ambaye pia alikuwa na kigugumizi, wakamwomba aweke mkono wake juu ya huyo mtu na amponye.

33 yBaadaye Isa akampeleka yule kiziwi kando mbali na watu, Isa akatia vidole vyake masikioni mwa yule mtu. Kisha akatema mate na kuugusa ulimi wa yule mtu. 34 zNdipo Isa akatazama mbinguni, akavuta hewa ndani kwa nguvu akamwambia, “Efatha!” Yaani, “Funguka!” 35 aaMara masikio yake yakafunguka na ulimi wake ukaachiliwa, akaanza kuongea sawasawa.

36 abIsa akawaamuru wasimwambie mtu yeyote habari hizi. Lakini kadiri alivyowazuia, ndivyo walivyozidi kutangaza kwa bidii. 37 acWalistaajabu mno. Wakasema, “Amefanya mambo yote vizuri mno! Amewawezesha viziwi wasikie na bubu waseme!”
Copyright information for SwhKC